Lissu amtaja mbunge wa CCM aliyemkodishia Ndege

Jumanne , 15th Sep , 2020

Mgombea Urais kupitia CHADEMA Tundu Lissu amesema kuwa mbunge wa jimbo la Mpendae Salim Turky aliyefariki dunia usiku wa kuamkia leo, ndiye aliyetoa fedha za kulipia gharama za Ndege iliyokodishwa kwa ajili ya kumpeleka Lissu kupatiwa matibabu nchini Kenya baada ya kushambuliwa kwa risasi.

Kushoto ni marehemu Salim Turky na kulia ni Tundu Lissu

Lissu ametoa kauli hiyo hii leo Septemba 15, 2020, wakati wa mkutano wake wa kampeni mkoani Njombe.

"Usiku wa kuamkia leo aliyekuwa mbunge wa Mpendae Salim Turky amefariki dunia, siku ile ya Septemba 7 niliposhambuliwa viongozi wangu wakasema lazima nipelekwe Nairobi, Salim Turky mwana CCM akamwendea Mwenyekiti Mbowe akamwambia, mimi nitatao Dola za Marekani laki moja ili Ndege ipatikane impeleke Lissu Nairobi", amesema Lissu.

Aidha Lissu ameongeza kuwa, "Kwahiyo ile Ndege iliyonipeleka Kenya usiku ule wa Septemba 7 mwaka ule ililipiwa na marehemu Salim Turky, mbunge wa CCM alikuwa ni mtu mwema sana, naomba tumkumbuke mtu huyo mwema, tumuombee apumzike kwa amani".

Salim Turky amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Septemba 15, 2020, na atazikwa jioni ya leo jioni huko Fuoni Kijito Upele Mkoa wa Mjini Magharibi.