Jumatatu , 18th Mar , 2019

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hammad amesema kuwa kwa mujibu wa utafiti walioufanya wamegundua kuwa Katiba ya Chama cha ACT-Wazalendo ndiyo pekee yenye masharti mepesi kwao.

Maalim Seif akiwa na Zitto Kabwe, kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo.

Maalim Seif ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wanahabari muda mfupi baada ya Mahakama Kuu kanda ya Dar es salaam, kukubali uamuzi wa msajili wa vyama vya siasa kumtambua Lipumba kuwa mwenyekiti wa chama cha wananchi (CUF).

''Mzigo wa CUF tumeutupa, hatuna habari tena na chama hicho, mambo hayo yamekwisha, sasa ni kusonga mbele na ACT Wazalendo, tumechambua vyama vyote na tukapitia Katiba zote, tukaona masharti ya ACT- Wazalendo, sio magumu na wametukaribisha vizuri'', amesema Maalim.

Sakata la Maalim Seif na Lipumba lilikotokea

Kabla ya hukumu ya leo Machi 18, 2019 kwenye kesi ya Chama Cha Wananchi CUF (upande wa Lipumba na Maalim Seif) ilihairishwa mara nne, mara ya kwanza ilikuwa Oktoba 10, 2018, ikapangiwa Novemba 30, 2018, ikaahirishwa hadi Januari 15, 2019, ikipangiwa tena Februari 22, 2019.