Jumanne , 18th Oct , 2016

Waziri wa TAMISEMI George Simbachawene amesema ni vigumu kwa madeni ya walimu kumalizika kabisa kwa sababu kila siku yanazaliwa madai mapya kutokana na shughuli zao za kila siku.

Waziri wa TAMISEMI George Simbachawene

Simbachawene ameyasema hayo alipokuwa akizungumza katika kipindi cha EAST AFRICA BREAK FAST kuifafanua kuhusu tishio la chama cha walimu nchini kuitisha mgomo nchi nzima kushinikiza serikali kuwalipa madeni yao.

“Mimi sijasikia tangazo lao la mgomo ila kusema kweli hakuna siku madeni ya walimu yataisha kabisa, tunachokifanya kwa sasa ni kumalizia uhakiki na kwenye uhakiki unakuta walimu wanaonesha wanaidai serikali ila ukiangalia na kukagua wengine wanakimbia, ila tukimaliza tutalipa kulingana na bajeti” Amesema Simbachawene.

Aidha Waziri amesisitiza kuwa changamoto ya walimu kukimbia zoezi la uhakiki husababisha muda kutumika zaidi kwa kuwa serikali haiwezi kutoa fedha zake bila kufanya uhakiki wa kina.

Pamoja na hayo Rais wa Chama cha Walimu nchini (CWT) Gratian Mukoba amesema serikali isipojitokeza hadharani na kutaja ni lini watayalipa, wataitisha mgomo nchi nzima.