Jumatatu , 12th Oct , 2020

Mgombea urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt John Magufuli amemuomba Mungu amsamehe aliyewahi kuwa Meya wa Ilala na baadaye kuhamia, CCM, Omary Kumbilamoto, kwani kipindi yupo CUF alikuwa anafanya hujuma kwenye maendeleo kwa lengo la kutoipa kiki serikali.

Kushoto ni mgombea urais kupitia CCM Dkt John Magufuli na kulia ni aliyekuwa Meya wa Ilala Omary Kumbilamoto

Magufuli ametoa kauli hiyo hii leo Oktoba 12, 2020, akiwa jimbo la Segerea wakati akiomba kura muda mchache tu baada ya Kumbilamoto kukiri makosa yake na kuomba msamaha.

"Ninamshukuru Meya aliyekuwa wa chama kingine aliyeokoka na kurudi CCM, ameeleza wazi kwamba walipoingia madarakani kazi yao kubwa ilikuwa ni kukwamisha maendeleo ya wana Dar es Salaam, nimesikitika sana, kwa sababu nilikuwa najua ninamshukuru sababbu amekiri na kutubu naomba Mungu amsamehe kwa dhambi alizozifanya", amesema Dkt Magufuli.

Awali Kumbilamoto wakati akiomba msamaha aliitaja miradi ambayo yeye kama mpinzani alishiriki kuihujumu ikiwepo ya soko la Kisutu, machinjio ya Vingunguti pamoja na hospitali ya Kivule

"Kabla sijaongea, nichukue fursa hii kwanza kukuomba msamaha wewe binafsi, CCM na wananchi kwa ujumla kwa mabaya tuliyowafanyia wakati tupo upinzani, nisikufiche Mheshimiwa Rais, miradi hii ilikwama kwa maelekezo kwamba tukiifanya sisi kama UKAWA tutakupa kiki ilibidi na sisi tutii, tukakuhujumu", amesema Kumbilamoto.