Magufuli azindua ujenzi wa 'fly over' Tazara DSM

Jumamosi , 16th Apr , 2016

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameweka jiwe la msingi katika ujenzi wa barabara ya juu (Fly Over) kwenye makutano ya barabara za Mandela na Nyerere eneo la Tazara jijini Dar es salaam.

Ujenzi huo wa barabara hiyo ya juu unatarajia kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 100 ambapo inajengwa kwa ushirikiano wa serikali ya Japan na Tanzania ambapo Tanzania ikichangia Bilioni 8.36 na Japan Bilioni 93.44.

Akizungumza katika shughuli hiyo Rais Dkt. Magufuli amewataka raia watakao ajiriwa katika mradi huo wawe waaminifu na kujiepusha na wizi wa mafuta kufanya migomo au wizi wa vifaa vya ujenzi.

Rais pia ametoa shukrani kwa serikali ya Japan kwa kuendelea kuisaidia Tanzania bila kuweka masharti magumu kama walivyo baadhi ya wafadhili.

''Ni bora kula muhogo wa kujitafutia mwenyewe kuliko kula mkate wa masimango'' Amesema Rais Magufuli.

Aidha akitoa salamu za Mkoa wa Dar es salaam Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda amemuhakikishia Rais Magufuli kwamba viongozi ambao wapo chini yake wapo tayari kumuunga mkono katika jitihada za kuleta maendeleo ya taifa.