Jumapili , 25th Jul , 2021

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Prof. Abel Makubi amesema muongozo wa kujikinga na Corona unataka mahabusu anayeingia kwa mara ya kwanza gerezani ni lazima apimwe Corona.

Picha ya gereza

Agizo hilo amelitoa leo Julai 25, 2021 ambapo amegusa maeneo mbalimbali ikiwemo miongozo shuleni, daladala, misiba, matamasha ya muziki na michezo.

“Mahabusu wote wanaoingia gerezani kwa mara ya kwanza au mtu aliyehukumiwa lazima apimwe kabla ya kuingia gerezani, lakini pia ndugu watakaokwenda kusalimia magerezani ataingia mmoja mmoja” - Prof. Abel Makubi Katibu Mkuu Wizara ya Afya.  

Kwa upande wa elimu amesema, “Shuleni tumetoa muongozo wanafunzi kuanzia miaka 8 watavaa barakoa endapo hawana magonjwa yanayowazuia kufanya hivyo wale ambao wako chini ya miaka 8 watazingatia taratibu zingine kama kunawa mara kwa mara''- Prof Abel Makubi Katibu Mkuu Wizara ya Afya. 

Aidha kwa upande wa mikusanyiko ya matamasha na michezo Prof Makubi amesema, “Matamasha ya Michezo, Muziki na mengine lazima yapewe vibali, michezo yote ya Mpira tulitoa muongozo tunaomba muongozo ufuatwe ikiwa ni pamoja na kukaa umbali wa mita moja baina ya shabiki na shabiki”- Prof. Abel Makubi Katibu Mkuu Wizara ya Afya.