Jumatatu , 9th Sep , 2019

Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Dar es Salaam,  imetoa maamuzi kesi ya maombi ya kupinga kuvuliwa ubunge iliyokuwa imefunguliwa na aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu, kwa kile kilichoelezwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo.

Tundu lissu

Maamuzi ya kesi hiyo yametolewa leo Septemba 9, 2019 na Jaji Sirillius Matupa na kudai kwamba kesi hiyo ni ya kikatiba hivyo inapaswa kufunguliwa kwa mfumo wa kesi ya uchaguzi na si kwa mfumo ambao alikuwa ameutumia,  huku pia akieleza kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kutengua ubunge wa Mbunge Julius Mtaturu aliyeteuliwa hivi karibuni.

Kesi hiyo namba 18 ya mwaka 2019, Lissu aliiomba Mahakama kibali cha kufungua shauri la kupinga taarifa ya Spika wa Bunge Job Ndugai ya kukoma ubunge wake,  ambapo Mahakama imetupilia shauri hilo.

Kwa upande wa waleta maombi katika kesi hiyo, wameahidi  kwamba watajipanga upya ili  kufungua kesi ya uchaguzi na hatimaye  kuipata haki yao. Hadi sasa Mbunge mteule wa CCM Julius Mtaturu, ataendelea kuwa Mbunge wa Singida Mashariki.