Jumatatu , 23rd Feb , 2026

Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, imeahirishwa hadi kesho baada ya Mahakama kushindwa kuendelea na usikilizwaji kufuatia mjadala mzito kuhusu notisi ya upande wa Jamhuri ya kuwasilisha ushahidi mpya.

Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, imeahirishwa hadi kesho baada ya Mahakama kushindwa kuendelea na usikilizwaji kufuatia mjadala mzito kuhusu notisi ya upande wa Jamhuri ya kuwasilisha ushahidi mpya.

Upande wa Jamhuri umeeleza kuwa uliwasilisha notisi hiyo Februari 20, 2026 kwa mujibu wa kifungu cha 308 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai. Wakili wa Serikali alidai kuwa notisi hiyo inaambatanisha maudhui (substance) ya ushahidi unaokusudiwa kuongezwa, ukiwa ni nyongeza ya ushahidi uliotolewa awali na ACP Amini Mahamba.

Kwa mujibu wa hoja ya Jamhuri, ushahidi huo unalenga kukidhi matakwa ya kifungu cha 308(1), huku kifungu cha 308(4) kikieleza kuhusu ushahidi uliopo kwenye jalada la kesi. Serikali ilidai kuwa ACP Mahamba alikuwa mchunguzi wa matukio yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi wa Oktoba 29, 2025, na kwamba maelezo hayo ni muhimu katika kuthibitisha hoja zao.

Hata hivyo, mshitakiwa Tundu Lissu alipinga vikali notisi hiyo akidai kuwa haikidhi matakwa ya kisheria. Alisema kifungu cha 308(1) kinahusu shahidi mpya ambaye ushahidi wake haukusomwa wakati wa hatua ya awali (committal proceedings), na kwamba upande wa Jamhuri hauleti shahidi mpya bali unataka kuwasilisha ushahidi wa ziada wa shahidi ambaye tayari alishatoa ushahidi wake katika hatua hiyo.

Lissu alieleza kuwa notisi hiyo si sahihi kisheria kwa kuwa haimtaji shahidi mpya kama inavyotakiwa, bali inalenga kuongeza ushahidi wa shahidi aliyekwisha kutoa ushahidi wake.

Aliongeza kuwa maelezo yaliyomo kwenye notisi yanayomtaja mchunguzi wa matukio ya uchaguzi mkuu wa 2025 hayapo kwenye hati ya mashtaka, na hivyo akadai kuwa upande wa Mashtaka unaonekana kutaka kubadilisha hati ya mashtaka kinyemela.

Aidha, Lissu alihoji uhalali wa kuingiza hoja za matukio ya Oktoba 29, 2025 akisema kuwa wakati huo alikuwa mahabusu kwa miezi sita na nusu.

Amesisitiza kuwa Mahakama ikiruhusu notisi hiyo, itakuwa imefungua “sanduku la Pandora” kwa kuruhusu masuala ambayo hayamo kwenye mashtaka kuingizwa katika kesi hiyo.

Akijibu pingamizi hilo, upande wa Mashtaka ulisisitiza kuwa notisi yao ipo kwa mujibu wa kifungu cha 308 na kwamba kuipinga ni sawa na kupinga ushahidi katika hatua ya committal.

Upande wa Jamhuri umedai kuwa ushahidi huo ni muhimu na haukusomwa wakati wa committal, hivyo unapaswa kuruhusiwa ili kuisaidia Jamhuri kuthibitisha mashtaka yake.

Mashtaka pia yameeleza kuwa, kuwasilishwa kwa ushahidi huo kutampa mshitakiwa fursa ya kuwahoji mashahidi ipasavyo, na hivyo kuomba Mahakama iridhie notisi hiyo.

Kwa upande wake, Lissu alisisitiza kuwa kifungu cha 308 kinazungumzia shahidi mpya na si ushahidi mpya, huku akidai kuwa iwapo ushahidi unaopendekezwa hauhusishi shahidi mpya, basi hauna msingi wa kisheria.

Lissu amesisitiza kuwa mlango wa kupokea ushahidi wa ACP Amini Mahamba tayari umefungwa kwa mujibu wa kifungu cha 308, na kwamba iwapo upande wa Jamhuri unahitaji ushahidi mpya, basi unapaswa kuwasilisha shahidi mwingine kama sheria inavyoelekeza.

Baada ya hoja hizo za pande zote mbili, Mahakama imeahirisha kesi hiyo hadi kesho Jumanne kwa ajili ya uamuzi na kuendelea na mashahidi wengine.