Jumapili , 20th Jan , 2019

Mahakama ya Juu ya nchini DR Congo imemtangaza kiongozi wa Upinzani, Bw. Felix Tshisekedi kuwa mshindi wa uchaguzi wa Urais baada ya kutupilia mbali pingamizi la mpinzani wake, Martin Fayulu.

Mahakama hiyo ya Kikatiba nchini Congo imesema Tshisekedi alishinda kwa kupata kura nyingi zaidi ya wengine, hivyo kumaanisha Tshisekedi atachukua nafasi ya Rais Joseph Kabila katika hafla ya kuapishwa siku ya Jumanne.

Baada ya mahakama kusema kuwa pingamizi lake halina msingi, Martin Fayulu anayedai alishinda uchaguzi huo uliofanyika Desemba 30, 2018 amezitaka Jumuiya za kimataifa kutomtambua Tshisekedi kwani yeye ndiye mshindi halali.

Umoja wa Afrika(AU) ni moja ya Jumuiya zilizotaka matokeo hayo kutotangazwa huku Mwenyekiti Paul Kagame na Mwenyekiti wa Tume, Moussa Faki wakitegemewa kwenda DRC Jumatatu.