Jumapili , 26th Jan , 2020

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameviagiza vyombo vya Ulinzi na Usalama vihakikishe vinawalinda wafanyabiashara wa madini wanaofanya kazi zao kwa kufuata sheria na kujiepuka kamata kamata zisizo na tija.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Ametoa agizo hilo leo (Jamapili, Januari 26, 2020) wakati akifunga semina ya ushiriki wa vyombo vya Ulinzi na Usalama katika usimamizi na udhibiti wa rasilimali madini katika ukumbi wa Mtakatifu Gaspar jijini Dodoma.

 “Katika kipindi cha hivi karibuni kumejitokeza malalamiko mengi kutoka kwa wawekezaji na wadau wa madini kuhusu kukamatwa au kubughudhiwa bila sababu za msingi. Kutokana na hali hiyo, natumia nafasi hii kukemea suala la ukamataji holela wa wawekezaji au wadau wa madini pasipo kufuata taratibu”, amesema Majaliwa.

Waziri Mkuu amesema Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini ina ofisi mikoa yote ya Tanzania Bara, hivyo hakuna sehemu ambayo wanaweza kusema walikosa msaada wa kitaalamu.

Akizungumzia kuhusu suala la unyanyasaji wa wafanyakazi wazalendo amesema si suala la kufumbiwa macho kama ilivyo suala la usalama wa watenda kazi katika migodi.  

Hivyo, ni wajibu wetu kushirikisha wadau wote wanaohusika na masuala ya ajira, bima za wafanyakazi, afya za wafanyakazi na usimamizi wa stahiki za wafanyakazi kukaa kwa pamoja na kutatua changamoto hii ili isiendelee kukomaa.”, amesema.

Pia, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kumpongeza na kumshukuru Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa uthubutu mkubwa alioufanya ambao umeleta mageuzi makubwa katika Sekta ya madini. Awali, Waziri wa Madini Doto Biteko alisema lengo la semina hiyo ni kujenga uelewa wa pamoja kwenye masuala ya usimamizi wa sekta ya madini nchini.