Jumanne , 19th Feb , 2019

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu kifungo cha miaka 17 jela washtakiwa watatu akiwemo raia wa China, Yang Feng Glan (66) maarufu Malkia wa Tembo.

Yang Feng Glan (Malkia wa Tembo) mwenye asili ya China.

Akizungumza leo Jumanne Februari 19, 2019, hakimu mkazi mkuu wa mahakama hiyo, Huruma Shaidi amesema amewatia hatiani washtakiwa hao.

''Ushahidi unaonesha jinsi gani washtakiwa wote watatu walivyosaidiana kuhakikisha wanatafuta meno ya tembo sehemu mbalimbali na kuyasafirisha'' ameongeza jaji Shaidi.

Ameongeza "Ushahidi wote unaonyesha jinsi gani nyinyi( washtakiwa) mmefahamiana kwa muda mrefu".

Mahakama imeeleza kwamba ushahidi umetolewa na watu 11 wakiwemo wasafirishaji.

Kila mmoja atatumikia kifungo cha miaka 17 baada ya kupatikana na hatia ya kujihusisha na biashara ya meno ya tembo yenye thamani ya bilioni 13.

Mbali na Glan, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 21/2014 ambaye  ni Salvius Matembo na Philemon Manase.

Mnamo mwaka 2015, jopo maalum la maafisa wanyama pori nchini Tanzania liliwakamata Bi Feng miongoni mwa wengine walioshukiwa kusafirisha pembe za ndovu.