Mfanyabiashara Mo Dewji akiwa na Haji Manara.
Taarifa za kutekwa kwa mfanyabiashara huyo anayekadiriwa kuwa na utajiri wa Sh3.5 trilioni zilianza kusambaa Alhamisi ya Oktoba 11, saa 1:00 asubuhi katika mitandao ya kijamii, kabla ya polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam kuthibitisha saa mbili asubuhi.
Akithibitisha kukamatwa kwa idadi ya watu hadi Jumapili Oktoba 14 katika mahojiano na www.eatv.tv kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema kuwa idadi imeongezeka na kufikia 26 na uchunguzi bado unaendelea.
"Mpaka sasa wanashikiliwa watu 26, na bado uchunguzi unaendelea endapo idadi ikiongezeka au kupungua tutawajuza", amesema Mambosasa.
Mapema Oktoba 11, baada ya kuenea kwa taarifa za kutekwa kwa mfanyabiashara huyo, Manara alinukuliwa akisema taarifa ya Mo kupata matatizo imemshtua kila mmoja na kwamba bado wanaliachia jeshi la polisi kufanya kazi yake kumpata mwekezaji wao. “Wanasimba wawe watulivu wakiliachia jeshi la polisi kufanya kazi yake na tunaamini MO atapatikana akiwa hai,” alisema Manara.
Kwa mujibu wa Kamanda Mambosasa amesema Manara anashikiliwa kutokana na kusambaza taarifa za tukio hilo kwenye mitandao ya kijamii kwa madai ya kutumwa na familia, jambo ambalo si la kweli.