Jumatatu , 20th Jul , 2020

Mkuu wa Mkoa wa Mara Adam Malima, amewataka vijana na wanaume ndani ya Mkoa huo kuhakikisha wanatimiza ahadi zao kwa wanawake ili waepukane na matukio ya wao kukatwa sehemu zao za siri na wanawake hao pindi wanaposhindwa kutimiza ahadi za kile walichokubaliana awali.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima.

Malima ametoa kauli hiyo hii leo Julai 20, 2020, kwenye kipindi cha SupaBreakfast ya East Africa Radio, hii ni baada ya John Lugera ambaye ni mkazi wa Tarime, kutoa malalamiko hayo kwenye kipindi hicho na kueleza kuwa wanaume wamekuwa wakikatwa sehemu za za siri na wanawake.

 "Huku kunakuwa na mauaji mengi, nilishawahi kushuhudia watu wameuana kwa sababu walikuwa wanadaiana Sh 2000, bado huku tuna hulka ya hasira za haraka haraka, lakini naona hapa mambo ni mawili badala ya kutafuta ajira yenye heshima anauza mwili wake", amesema RC Malima.

"Kuna ahadi hapo waliwekeana zinavunjwa na hao wanaume wanapokwenda huko wakikubaliana watimize ahadi za watu" ameongeza RC Malima.

Awali akitoa malalamiko hayo, mwananchi huyo alisema kuwa "Huku mkoani Mara matukio yanayoendelea ni ya wanawake kukata sehemu za siri za wanaume, mfano mwanamke umeingia naye sehemu mliaahidiana kumpa elfu 10, halafu ukampa elfu 5, usipompa yote anakukata sehemu zako za siri", amesema John Lugera.