Jumanne , 1st Nov , 2022

Wizara ya mambo ya nje ya nchini Korea Kaskazini imeikosoa nchi ya Marekani kwa kutanua luteka za pamoja za kijeshi na Korea Kusini ambazo inadai ni mazoezi yanayolenga kufanya uvamizi. 

Kifaru cha kivita

Korea Kaskazini imetahadharisha itachukua hatua kali kujibu luteka hizo. 

Taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Korea Kaskazini imetolewa wakati Marekani na Korea Kusini zikifanya luteka za angani zinazohusisha ndege za kivita zaidi ya 200, zikiwemo ndege chapa F-35, wakati zinapoimarisha mifumo yao ya ulinzi kufuatia hatua ya Korea Kaskazini kuendelea kufanya majaribio ya makombora na kuongezeka kwa kitisho cha nyuklia.

Washington na Seoul siku ya Jumatatu zilianza moja ya mazoezi yao makubwa zaidi ya kijeshi ya anga, ambayo yatakamilika Ijumaa ya wiki hii.

Korea Kaskazini pia imerusha mfululizo wa makombora katika wiki za hivi karibuni kujibu mazoezi mbalimbali hii inafuatia ripoti za kijasusi kwamba Pyongyang inajiandaa kwa jaribio la kwanza la silaha za nyuklia tangu 2017.