Jumatatu , 4th Oct , 2021

Mdau wa masuala ya elimu nchini na mwandishi wa vitabu, Richard Mabala, amesema kuwa ili kuona wanafunzi wanaojiamini basi haina budi masomo kama Physics, Biology na History yakafundishwa kwa lugha ya Kiswahili ili kutoa nafasi ya wanafunzi kuyaelewa vizuri zaidi.

Mwandishi wa vitabu, Richard Mabala

Kauli hiyo ameitoa hii leo Oktoba 4, 2021, wakati akizungumza kwenye kipindi cha Supa Breakfast cha East Africa Radio na kusisitiza kwamba Kiingereza kifundishwe vizuri zaidi kama somo ili kieleweke kwa ufasaha na si masomo kufundishwa kwa kutumia lugha hiyo.

"Physics na Historia waijue kwa Kiswahili, ndiyo wataelewa vizuri na mtihani utolewe kwa Kiswahili na hapa ndiyo utaona wanafunzi wetu wengi sana hawastahili kupata sifuri, wana uwezo, na akili na tutaona wanafunzi wanaojiamini sababu wamelelewa katika elimu inayowapa nafasi ya kujadili, kutumia uwezo wao wa kufikiri na ubunifu," amesema Mabala.