
Mawaziri hao wa fedha na magavana wa benki kuu kwenye mkutano huo wa G-7, mbali na kuzungumzia juu ya kuiunga mkono Ukraine inayokabiliwa na vita pia kwenye ajenda ya mkutano wao wanaangazia wasiwasi wa kutokuwepo na uhakika katika shughuli za mabenki pamoja na kusambaratika baadhi ya mabenki nchini Marekani na vilevile hofu ya taifa hilo kubwa kushindwa kulipa deni lake la taifa.
Rais wa benki kuu ya Umoja wa Ulaya, ECB Christine Lagarde amesema jumuiya hiyo inachukua hatua za kukabiliana na Benki Kuu ya Umoja wa Ulaya mwezi huu iliamua kubadili sera yake na kuongeza viwango vya riba kwa mara ya saba mfululizo, ingawa ongezeko hilo limepungua kutoka asilimia 0.5 hadi asilimia 0.25.
Wakati huo huo kundi hilo la nchi saba tajiri linatarajiwa kutoa tamko jinsi ya kuishughulikia China. Chanzo kimoja cha serikali ya Ujerumani kimesema wanachama wa G-7 wanatarajiwa kusema wamekubaliana kwa pamoja kwamba lengo la mataifa hayo si kuanzisha muungano wa kupambana na China katika mradi wake wa kimataifa wa miundombinu bali ni kutafuta njia za kuanzisha mradi mbadala kama huo utakaodhibiti uwekezaji wa China.
Waziri wa fedha, Shunichi Suzuki wa Japan ambayo ni mwenyeji wa mkutano huo amesema nchi yake itazindua mpango juu ya kuhamasisha uchangishaji wa dola bilioni 1 kwa ajili ya kuzisaidia nchi zinazoizunguka Ukraine ili ziweze kuwapokea wakimbizi kutoka kwenye nchi hiyo iliyokumbwa na vita.