Jumatatu , 8th Apr , 2019

Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko amemjia juu aliyekuwa Hakimu wa kesi inayomkabili yeye pamoja na viongozi wa juu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Jaji Wilbard Mashauri ambapo amedai ilikuwa ni mpango ili wao kukaa rumande kwa zaidi ya miezi 3.

Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara mkoani Tarime Esther Matiko pia ametoa shukrani kwa Jaji Rumanyika aliyewapatia dhamana na kusema licha ya kukaa rumande kwa muda mrefu alijifunza jinsi watuhumiwa wanavyoishi.

"Wote tunajua masharti ya dhamana, kuna Mahakimu wengine wanaendeshwa. Hakimu Mashauri namtaja bila kuogopa na amebakisha mwaka mmoja kustaafu lakini sasa hivi amekuwa Jaji, ila namshukuru Jaji Rumanyika alieleza hukumu yake na kuweka mwanzo mzuri kwa Watanzania." amesema Matiko

"Kwa upande mwingine ilikuwa ni neema kwangu, mimi nilivyoenda Segerea nimeona mengi, kwa hiyo nitaendelea kuwatetea watanzania wengine, japo kwa sasa CCM wameanza kupiga propaganda eti nataka kuhamia Kinondoni", ameongeza Matiko.

Mbowe na Matiko walikaa rumande kwa zaidi ya miezi mitatu baada ya kukiuka masharti ya dhamana waliyopewa  na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Novemba, 2018.