Matumizi ya 'Antibiotics' yanavyoweza kuacha sumu

Ijumaa , 16th Nov , 2018

Watu wametakiwa kuwa makini na matumizi ya dawa hususani 'Antibiotics' bila kufuata ushauri wa daktari, jambo ambalo ni hatari kwani hutengeneza sumu mwilini kutokana na dawa hizo kuwa na kemikali sumu ambazo hupambana na bakteria.

Antibiotics

Akizungumza kwenye MJADALA wa East Africa Television, Mtaalam wa Afya kutoka Hospitali ya taifa Muhimbili Ruchius Philbert amesema kuwa imekuwa ni tabia ya wengi kunywa dawa kwa mazoea lakini madhara yake ni makubwa.

"Dawa za Antibiotic hazitibu magonjwa yote kama wengi wanavyodhani kuwa dawa hiyo ina msaada kwenye kila ugonjwa, na kuna wakati dawa hizi zikitumika ovyo husababisha kuua baadhi ya bakteria wanaolinda kinga mwilini", amesema .

Ameongeza kuwa bila kufanya vipimo na kujua mgonjwa anaumwa ugonjwa gani, kuna hatari ya kutumia dawa ambazo mwisho zitakosa vimelea vya ugonjwa wa kupambana nao na mwisho kutengeneza sumu ambayo ni hatari zaidi kwa kinga ya mwili.

Tanzania na dunia kwa ujumula ipo kwenye maadhimisho ya wiki ya matumizi ya dawa za 'Antibiotiki' ambapo Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto inatoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi sahihi ili kuepusha ongezeko la magonjwa yanayosababishwa na matumizi mabaya ya dawa.