Jumatano , 12th Oct , 2016

Serikali imesema itawachukulia hatua madereva wa malori ya mchanga na kokoto wasiofuata sheria za ubebaji wa bidhaa hiyo na kusababisha uharibifu wa miundombinu ya barabara.

Prof Mbarawa katika ukaguzi wa ujenzi wa moja ya barabara nchini.

Tamko hilo limetolewa leo na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa na kutoa agizo kwa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), kushirikiana na Jeshi la polisi pamoja na wananchi kuwabaini madereva wa aina hiyo.

Waziri Mbarawa ametoa agizo hilo mkoani Kigoma katika ziara yake ya kukagua barabara ya Kidahwe-Kasulu yenye urefu wa kilometa 50 ambapo pamoja na mambo mengine amesema Serikali inatumia fedha nyingi kujenga miundombinu ya barabara kwa maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla hivyo haitamvumilia mtu yeyote atakayebainika kuharibu miundombu hiyo kwa makusudi.

Aidha, Profesa Mbarawa ameliomba Jeshi la Polisi kushirikiana vyema na wakandarasi wanaojenga miundombinu ya barabara katika maeneo mbalimbali nchini kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria baadhi ya watu wasio waaminifu ambao wanaiba vifaa vya wakandarasi jambo linalochangia kukwamisha shughuli za ujenzi wa barabara.

Naye Meneja wa TANROADS mkoa wa Kigoma Eng. Narcis Choma, amebainisha changamoto zinazokabili mradi huo kuwa ni wizi wa mafuta na vifaa vya ujenzi hali inayosababisha mradi kusuasua.

Kwa upande wake Mhandisi Mkazi Mekbib Tesfaye anayesimamia mradi huo kutoka Kampuni ya DOCH Limited, amesema kuwa mradi huo umefikia asilimia 24 ambapo kwa sasa kazi inayofanyika ni ujenzi wa madaraja mawili na makalvati katika barabara hiyo.

Katika hatua nyingine, Waziri Prof. Mbarawa ametembelea Chuo cha Mamlaka ya Hali ya Hewa Mkoani Kigoma na kuahidi uongozi kuwa atazishughulikia haraka changamoto kadhaa zinazokikabili chuo hicho ili kuweka mazingira rafiki ya kujisomea kwa wanafunzi wanaosomea taalauma hiyo.