Jumatano , 21st Aug , 2019

Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, amewataka wakuu wa nchi 16 zinazounda Jumuiya ya SADC, katika mkutano ujao kufikiria kuja na ajenda ya pamoja, juu ya kuwa na sera ya pamoja ya elimu kwa nchi wanachama.

Mbatia ametoa kauli hiyo baada ya kumalizika kwa ibada ya misa takatifu ya Jubilee ya fedha ya miaka 25 ya Padri Thomas Salekio Kessy, iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Yohana mkoani Kilimanjaro.

Mbatia amesema kuwa, "majuzi nilisikia na kusoma baadhi ya maandiko kwamba watu Wanamibia wao wanasema mwanafunzi anayetoka Tanzania, amemaliza kidato cha sita akienda kwao, kupata Chuo Kikuu kule ni shida, kwa sababu Namibia wao mfumo wao ni mgumu, wao elimu zao wanamalizia kidato cha nne.

"Unajiuliza silabasi zetu zimeundwa namna gani, nawashauri wakuu wa nchi wanachama ni vizuri tukawa na sera moja ya SADC katika masuala ya elimu,” amesema Mbatia.

Mwaka huu Tanzania imekuwa mwenyeji wa mkutano wa 39 wa SADC, ikiwa imepita miaka 16, tangu mkutano kama huo kufanyika kwa mara ya mwisho mwaka 2003, chini ya utawala wa Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa.