Ijumaa , 15th Mar , 2019

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Freeman Mbowe amesema uamuzi uliofanywa na Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa wa kukihama chama hicho yalikuwa ni maamuzi yake binafsi.

Freeman Mbowe ametoa kauli hiyo Jijini Dar es salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya hali ya siasa nchini ambapo kwa sasa amesema amefunga mjadala wa kiongozi huyo.

Mbowe amesema, "kuhusu aliyekuwa mgombea wetu 2015, Edward Lowassa baada ya kurudi CCM, vyama vyote vinakusanya watu kwa mahitaji maalumu na watu hao wanakuwa na mambo yao pengine kutaka kuwatumikia watu au tamaa ya madaraka".

Kuhusiana na kukaa magerezani kwa muda mrefu Mbowe amesema, "kuna ugonjwa uliopo magereza kwa lugha ya huko unaitwa 'Burudani' ambao ni ugonjwa wa ngozi na unaambukiza, chanzo chake ni Kunguni na Chawa".

Mbowe pamoja na Mbunge wa Tarime Mjini Esther Matiko wamekaa kwa zaidi ya miezi 3 gerezani kutokana na kosa la kukiuka masharti ya dhamana.