Jumatatu , 14th Mar , 2016

Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Mhe. Freeman Mbowe ameweka wazi sababu za chama hicho kimemteua Dkt. Vicent Mashinjji kuwa katibu Mkuu mpya wa Chama hicho.

Katibu Mkuu mpya wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dkt. Vicent Mashinji.

Akiongea jana katika Mkutano wa hadhara wa kumtambulisha katibu mkuu huyo jijini Mwanza katika Viwanja vya furahisha Mhe. Mbowe amesema sifa na uwezo wake wa kimkakati katika kuimirisha chama ndiyo sababu kubwa iliyofanya waweze kumteua Dkt. Mashinji.

Kwa upande wake Katibu Mkuu huyo Mpya akiongea na wananchi waliojitokeza katika utambulisho wake huo amesema kuwa jukumu lake la kwanza ni kujenga chama kimkakati zaidi ili kiweze kusonga mbele.

Aidha amesema kuwa dhamira yake kubwa ni kuona katiba, Sheria na maamuzi ya wananchi yanafuatwa ikiwa ni pamoja na kudumisha amani na utulivu huku akisema kuwa uongozi wake utagatua zaidi madaraka kwa wananchi.

Nae aliyekuwa Mgombea urais wa Chama hicho kupitia mwamvuli wa UKAWA,Mhe. Edward Lowassa amewashukuru wananchi wa Mwanza kwa kura walizompigia lakini akasisitiza kuwa safari ya mabadiliko imeanza tena rasmi kupitia katibu mkuu huyo Mpya.