Jumatatu , 18th Jun , 2018

Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe amelazwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili baada ya kudondoka ghafla alfajiri ya leo kwa mujibu wa wakili wake Jeremiah Mtobesya.

Wakili wa Mbowe, aliiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mbele ya Hakimu Mkazi mkuu, Wilbard Mashauri, kuwa mteja wake alianguka leo Juni 18 akiwa nyumbani kwake hivyo asingeweza kufika mahakamani kwa siku ya leo.

Akiwasilisha taarifa hiyo, Wakili Mtobesya ameeleza kuwa Mbowe ambaye ni mshtakiwa namba moja katika kesi namba 112 ya 2018 amefiwa na kaka yake Henry Mbowe usiku wa kuamkia leo.

Awali Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi aliiambia mahakama kuwa kesi ilipangwa kwa ajili ya washtakiwa Mbowe na wenzake wanane kusomewa maelezo ya awali PH na kwamba wamejiandaa na wapo tayari.