Jumanne , 7th Mei , 2024

Uongozi wa Simba SC umesema utafanya usajili wa kishindo kwa ajili ya msimu ujao 2024-2025 kwa kusajili wachezaji wenye hadhi na uwezo mkubwa ili kutimiza malengo yao ya kurejesha mataji ndani ya viunga vya Msimbazi Jijini Dar es Salaam.

Akifanya mazungumzo maalum na EATV,Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba SC Ahmed Ally amesema kuwa mchakato wa kuboresha timu hiyo umeanza na tayari viongozi wameanza kusambaa nchi mbalimbali kusaka wachezaji huku wachezaji waliomaliza mikataba wanaotakiwa kusalia ndani ya timu wamesaini mikataba ya kusalia ndani ya Simba SC .

"Tetesi za usajili zimekuwa nyingi wale wachezaji wetu wazuri wanahusishwa kuondoka tupo kwenye mazungumzo na wachezaji ambao wanamaliza mikataba yao mchezaji yeyote tunayemhitaji atabaki na tusiyemhitaji hata kama ana mkataba tutamuacha,amesema Ahmed.

Kwa upande mwingine,Ahmedy Ally amesema kuwa wanaendelea kupokea barua za maombi ya kazi kutoka kwa makocha mbali mbali wakiomba kuifundisha timu hiyo na kudai kila kitu watakiweka wazi hapo baadae pamoja na kumtangaza mkufunzi mpya ndani ya wababe hao wa Msimbazi.