Jumatatu , 1st Apr , 2019

Mbunge wa Arumeru Magharibi kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Gibson Meiseyeki amemjia juu Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Muro na kueleza kuwa haihitaji kuonekana na kiongozi huyo ili ijulikane anatekeleza majukumu ya kibunge.

Meiseyeki ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na www.eatv.tv iliyotaka kufahamu juu ya kauli ya Mkuu wa Wilaya Arumeru wakati akizungumza na East Africa Breaksfast ya East Africa Radio ambapo alidai tangu ateuliwe na Rais Magufuli hajawahi kukutana na Mbunge Mbunge wa Jimbo hilo jimboni kwake.

Akijibu madai hayo ya kutoonekana jimboni Meiseyeki amesema kuwa, "mimi sio Baba mkwe wake wala hajaoa kwetu kwa hiyo haitaji kuniona ili kutekeleza majukumu yake, afanye ya kwake na mimi nifanye ya kwangu,".

"Mimi ni mwakilishi wa wananchi labda tubadilishane mimi niwe Mkuu wa Wilaya, yeye awe Mbunge, na ofisi yangu kwa sasa iko Dodoma sio wilayani, haihitaji kuniona mimi nikimaliza vikao huwa narudi nyumbani kwangu Arumeru, kwa hiyo akisema hajaniona hajaamua kunitafuta."

Hivi karibuni pia wakati akizungumza na www.eatv.tv, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Jerry Muro alizungumzia juu ya madai kutamani Ubunge katika Jimbo la Hai ambalo kwa sasa linaongozwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Freeman Mbowe.