Jumatatu , 23rd Sep , 2019

Serikali kupitia Wizara ya Maji imetenga kiasi cha Shilingi bilioni 2 kwa ajili ya kutatua kero ya maji katika jimbo la Mbunge wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu, baada ya Rais Magufuli kuagiza changamoto hiyo ishughulikiwe mapema.

Akizungumza leo na EATV & EA Radio Digital, Septemba 23, 2019 Mtaturu amesema kuwa amefurahishwa kuona serikali imechukua hatua za haraka kuishughulikia changamoto hiyo, ambapo hadi sasa vimekwishachimbwa visima 28 watakavyotumika kusambaza maji jimboni humo.

''Bahati nzuri niliongozana na Naibu waziri wa Maji kwa maelekezo ya Wizara na Mh Rais, kwamba aje tuangalie changamoto ya maji pamoja. Nashukuru kwamba wizara imetupataia bilioni 2 na imewaacha wataalamu wa maji hapa ili kuangalia namna ambavyo watazigawa hizo pesa katika maeneo ambayo yalikuwa na changamoto'', amesema Mtaturu.

Ameongeza kuwa mbali na changamoto ya maji jimbo lake linakabiliwa na changamoto ya ubovu wa miundombinu ya barabara na kuleta adha kubwa kwa watumiaji, hususani wakulima wakati wa kusafirisha mazao yao na kwamba Wizara ya ujenzi imemuahidi kutafuta fedha.