Alhamisi , 8th Oct , 2015

Mgombea ubunge jimbo la Iringa mjini kupitia (CHADEMA), Mch. Peter Msigwa na wafuasi wengine watatu wa chama hicho wamefikishwa mahakamani na kusomewa mashitaka yanayohusiana na uvunjifu wa amani pamoja na kuwashambulia askari wa jeshi la polisi.

Mgombea Ubunge jimbo la Iringa Mjini Mchungaji Peter Msigwa akiongea na Waandishi wa Habari mara baada ya kutoka Mahakamani Jana

Mchungaji Msigwa na wenzake watatu wamefikishwa mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya mkoa wa Iringa David Ngunyale na kusomewa mashitaka manne yakufunga barabara na kusababisha uvunjifu wa amani,kuharibu gari ya jeshi la polisi pamoja na kuwashambulia na kuwajeruhi askari polisi wawili akiwemo kamanda wa kikosi cha kutuliza ghasia mkoani iringa.

Washitakiwa hao wanne ni sehemu tu ya watuhumiwa kumi wanaotuhumiwa kwa vurugu hizo zilizotokea siku ya tarehe 28 mwezi septemba, ambapo awali taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na kamanda wa polisi mkoani Iringa Ramadhani Mungi iliwatuhumu wafuasi wa chadema kwa kufunga barabara na kuwafanyia vurugu wafuasi wa Chama cha Mapinduzi waliokuwa wametokea kwenye mkutano wa mgombea urais kupitia chama chao uliofanyika kwenye uwanja wa Samora

Washitakiwa wote wameachiwa kwa dhamana mpaka kesi yao itakapotajwa tena Novemba 2 mwaka huu ambapo mgombea ubunge wa jimbo la iringa mjini Mchungaji Peter Msigwa amesema pamoja na mashitaka hayo wanachadema hawapaswi kukata tamaa ya kufanya kampeni za amani ili kuhakikisha wanashinda.