Alhamisi , 30th Jul , 2020

Mchakato wa mchujo kwa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), walioomba kugombea Udiwani, unaanza leo kwa vikao vya chama hicho vya Kata kuwajadili wagombea. 

Bendera za CCM

Kwa upande wa wagombea Ubunge na uwakilishi kwa Zanzibar, vikao vya majimbo pia vinaanza leo, huku vikao vya Wilaya kwa upande wa Tanzania Bara, vinatarajiwa kuanza keshokutwa hadi Agosti 2, mwaka huu.

Tayari CCM imekamilisha mchakato wa kura za maoni kwa ngazi ya Ubunge, Udiwani na uwakilishi, ulioanza tangu Julai 14 na kukamilika Julai 17, mwaka huu, kwa mara ya kwanza katika historia ya CCM, kulikuwa na idadi kubwa ya wanachama waliojitokeza kuchukua fomu, kuomba kuteuliwa kugombea nafasi hizo, kwa ngazi ya Ubunge pekee, jimbo moja idadi ya chini ya wanachama waliojitokeza ilikuwa si chini ya watu 30.

Dar es Salaam kuna Wilaya tano na majimbo 10, ambapo Wilaya ya Ubungo ina majimbo ya Ubungo na Kibamba, Wilaya ya Kinondoni ina majimbo ya Kinondoni na Kawe na wilaya ya Temeke ina majimbo ya Mbagala na Temeke.

Aidha, wilaya ya Ilala ina majimbo ya Ilala, Segerea na Ukonga na Wilaya ya Kigamboni ina jimbo moja la Kigamboni. 

Baada ya vikao vya Kata kujadili wagombea wa udiwani, vitatoa mapendekezo kwa kamati za siasa za wilaya, ambazo zitatoa mapendekezo kwa Halmashauri Kuu za Mikoa ambazo zitajadili wagombea na kuteua wagombea wa udiwani mmoja katika kila kata mkoani humo. 

Kwa upande wa Ubunge, baada ya vikao vya wilaya kupendekeza majina ya wagombea watakaokiwakilisha chama hicho kwenye Uchaguzi Mkuu Oktoba 28, mwaka huu, maoni ya vikao hivyo yatawasilishwa kwa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM. 

Kamati hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Dkt John Magufuli itateua jina moja la mwana CCM ,atakayepeperusha bendera ya chama hicho kwenye uchaguzi wa mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.