Tamko la kufanya mgomo huo limetolewa na viongozi wa umoja huo wakiongozwa na Katibu wao Bw. Rashid Salehe, waliokutana na wanachama wao jijini Dar es Salaam leo, ili kupeana taarifa ya maazimio ya mkutano uliokuwa ufanyike April 18 mwaka huu baina ya wawakilishi wa madereva na serikali.
Mawaziri kutoka wizara za Kazi, Fedha, Uchukuzi, pamoja na Mambo ya Ndani ya Nchi, walikuwa wakutane na wawakilishi wa madereva hao, ili kujadili kero hizo ambazo ni pamoja na kutokwepo kwa mikataba ya ajira, amri ya kwenda kusoma kila wanapotaka kuhuisha leseni zao, pamoja na kero nyingine mbalimbali zinazohusu sekta ya usafiri ikiwemo wimbi la ajali za barabarani.
Mgomo huo upo dhahiri kutokana na ukweli kwamba ni vigumu kwa serikali kutatua kero za madereva hao ndani ya siku chache zilizobakia, ambapo katibu wa umoja huo Bw. Salehe amesema hivi sasa hawapo tayari kukaa vikao vingine na serikali zaidi ya kuitwa na kupewa majibu ya utekelezaji wa madai yao kwa vitendo.
Awali wakati akifungua mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa Kimara Resort jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa umoja huo Bw. Clement Masanja amesema inasikitisha kuona serikali imeshindwa kusikikiliza hoja za madereva na hasa ilivyoonesha dharau kwa kushindwa kukutana nao katika mkutano uliopangwa kufanyika April 18 mwaka huu.
Kwa mujibu wa Masanja, madereva wanashangazwa na kitendo cha Wizara ya Kazi na Ajira kukutana na wamiliki wa mabasi siku moja kabla ya April 18, kitendo wanachokitafsiri kuwa ni dharau na kuwepo kwa mazingira ya rushwa.
"Haiwezekani sisi ndio wenye malalamiko lakini badala ya serikali kukutana na kutusikiliza sisi kwanza, yenyewe inawaita na kujadiliana na wamiliki wa mabasi na malori ambao kimsingi ndio wenye mgogoro na sisi...kitendo hiki sio cha kiungwana na kimeonesha jinsi serikali yetu inavyokumbatia matajiri," alisema Masanja.
Ameongeza kuwa baada ya mawaziri wa wizara husika kutoonekana kwenye mkutano huo waliamua kumwandikia barua waziri Mkuu Mizengo Kayanza Pinda lakini katika hali ya kushangaza na yeye mpaka sasa hajachukua hatua yoyote, hali inayoonyesha kuwa ameridhishwa na utendaji wa mawaziri walio chini yake.
Kwa upande wake, Salehe amesema wanashangazwa na jinsi serikali kupitia mamlaka ya usafiri wa majini na nchi kavu - SUMATRA ilivyoshughulikia kwa haraka tishio la mgomo kutoka kwa wamiliki wa mabasi - TABOA kiasi cha kukutana hadi saa nane za usiku, lakini imeshindwa kushughulikia kero za madereva wa mabasi ambayo matajiri hao wa TABOA ndio wamiliki.
Kwa upande wake, makamu mwenyekiti wa umoja huo Bw. Shaban Mdemu amesema amelalamikia ukaguzi wa mara kwa mara unaofanywa na kikosi cha usalama barabarani kwa daladala jijini Dar es Salaam na maeneo mengine nchini kuwa ni wa usumbufu kwani ukaguzi huo ni sehemu tu ya ujanja ujanja wa kujipatia pesa kutokana na kutokwepo kwa utaratibu unaoeleweka.
Ametolea mfano pendekezo lao kwa mkuu wa kikosi cha usalama barabarani kuwa ingetengwa siku maalumu kwa daladala zote ziendelee kufanyiwa ukaguzi ili kuondoa usumbufu kwa madereva na abiria, lakini cha kushangaza, Mdemu amesema kuna wakati daladala moja hukaguliwa hadi mara kumi na nne kwa siku, kitendo alichodai kuwa ni usumbufu mkubwa kwa kazi yao.
Aidha, ameshangazwa na kitendo cha askari wa usalama barabarani kutumia vitabu vya faini vya zamani kwa makosa yanayofanyika hivi sasa, kitendo ambacho amekitaja kuwa ni aina nyingine ya ufisadi, kwani hana uhakika iwapo makusanyo hayo yanafikishwa serikalini kwani ana uhakika kuwa vitabu hivyo vimefutwa kutoka kwenye kumbukumbu ya hazina punde mwaka wake wa kutumika ulipoisha.