Jumamosi , 23rd Jun , 2018

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza mifumo ya utoaji huduma Serikali kwa njia ya mitandao isitumike kukwamisha shughuli za Serikali au mipango ya utoaji huduma kwa wananchi.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akisisitiza jambo.

Amesema watakaobainika kuhujumu mifumo hiyo wachukuliwe hatua za kinidhamu na amesisitiza kwamba Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli haitawavumilia watumishi wasio waadilifu.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo, Juni 23, 2018 mara baada ya kuzindua mifumo tisa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwenye kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwenye Viwanja vya Mwalimu Nyerere, jijini Dodoma. 

Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2018 iliyotolewa na Umoja wa Afrika (AU) ni, “Mapambano dhidi ya Rushwa kwa kushirikisha wadau na kujenga uongozi bora ili kufikia Malengo ya Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika na Malengo ya Maendeleo Endelevu” amesema Majaliwa.

Mifumo hiyo aliyoizundua inahusu utoaji Huduma Serikalini ambayo ni Mfumo wa Usajili wa Vizazi  na Vifo, Mfumo wa Taarifa za Kitabibu, Mfumo wa Taarifa za Ununuzi, Mfumo wa Kumbukumbu za Kielektroniki na Mfumo wa Ofisi Mtandao.