
Endapo atashindwa mkataba wake utavunjwa.
Kufuatia hatua hiyo Wakuu wa wilaya za Mkinga, Korogwe na Pangani wamekubaliana kwa pamoja kumpa mwezi mmoja wa utekelezaji mkandarasi huyo
Hatua hiyo imekuja baada ya mradi huo kubainika umetekelezwa kwa asilimia 8 wakati kwa mujibu wa mkataba mradi huo ulitakiwa uwe umefikia asilimia 68
Mkuu wa Wilaya ya Mkinga Kanal Maulid Sulumbu ametoa kauli hiyo wakati akitoa taarifa ya maazimio ya kikao cha pamoja kilichoketi kujadili kasi ndogo ya mkandarasi huyo kwenye utekelezaji wa mradi huo katika wilaya hizo
Kanal Sulumbu amesema kuwa katika mazungumzo yao ya pamoja wamekaa na mkandarasi huyo na kumbana ambapo ameelezea changamoto zake ambazo wamezikubali na wakakubaliana kuanzia sasa mkandarasi aongeze kasi pamoja na nguvu kazi ili aweze kuwasha umeme katika vijiji 10 kila mwezi
"Baada ya kuona kazi ya mkandarasi huyu imezorota tumempa mwezi mmoja kutekeleza makubaliano haya na niseme tu kwamba serikali hairidhishwi na utekelezaji wa mradi unaofanywa na mkandarasi huyu, " alisema Kanali Sulumbu
Mkuu wa wilaya ya Korogwe Basila Mwanukuzi amesema kwa ujumla hawakuridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi huo wakati serikali kupitia Ilani ya CCM iliahidi kuwafikishia umeme wananchi wake jambo mkandarasi alifanya kwa kasi ndogo.
"Nataka niseme wazi hapa kwamba Wananchi wanamategemeo makubwa na serikali yao kupata umeme, mnavyochelewa namna hiyo mnapunguza kasi ya Maendeleo vijijini," amesema Mwanukuzi.
Akizungumza kwa niaba ya wabunge wa majimbo hayo matatu ikiwemo jimbo la Mkinga, Pangani na Korogwe, Mbunge wa jimbo la Mkinga Dastan Kitandula amesema kuwa kikao hicho kimetokana na kuzorota kwa mradi huo huku mkandarasi akitoa ahadi zilizoshindwa kutekelezeka.
Kitandula amesema tangu kuingia mkataba na kampuni hiyo serikali ilitoa fedha kiasi cha shilingi bilioni 3 mwezi February mwaka jana lakini kampuni hiyo haijafanya lolote.
Amesema lengo la kikao hicho ni kutatua mkwamo na mwenendo wa mradi huo baada ya ahadi mbalimbali ambazo mkandarasi amekuwa akizitoa siku za nyuma.
"Ahadi iliyotolewa na serikali ni kupeleka umeme kwa wananchi leo hii mlipaswa muwe mmetekeleza mradi kwa asilimia 68, lakini hadi sasa mmetekeleza kwa asilimia 8 tu, kiukweli haturidhishwi," alisema Kitandula.
Kitandula alisema mradi huo wa umeme katika wilaya ya Korogwe unatekelezwa katika Vijijni 54, Mkinga Vijiji 23 na Pangani Vijiji 3.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa wakala wa nishati vijijini (Rea) Mhandisi Hassan Said amesema kuwa wametoa muda huo na kama mkandarasi atashindwa kutekeleza hatua stahiki zitachukuliwa.
Mkurugenzi huyo wa Rea amesema mkataba baina ya mkandarasi huyo ni wa miezi 18 tangu February mwaka jana.
"Mkandarasi atakuwa na option mbili, afanye mradi ili aendelee na kazi au ashindwe yale tuliyokubaliana sisi leo tuchukue hatua za kimkataba," alisema Mhandisi Saidy.
Hata hivyo Mkandarasi wa mradi huo John Zheng amesema yupo tayari kumaliza mradi huo kwa wakati baada ya changamoto ya iliyokuwa ikiwakabili ya ugumu wa uingizwaji wa baadhi ya vifaa.
Alikiri kuchelewesha mradi huo akidai baadhi ya vifaa vya mradi huo vinatoka nje ambako kutokana na vita vya Urusi na Ukraine vimeshindwa kufika kwa wakati.
Mradi huo utagharimu jumla ya kiasi cha shilingi bilioni 22 na mpaka hivi sasa mkandarasi ameshalipwa kiasi cha shilingi bilioni 3