Mkapa apumzishwa rasmi kijijini Lupaso

Jumatano , 29th Jul , 2020

Safari ya Rais wa awamu ya tatu Benjamin William Mkapa, imefika tamati rasmi hii leo baada ya kupumzishwa katika nyumba yake ya milele kijijini Lupaso, Wilayani Masasi Mkoani Mtwara. 

Marais Wastaafu Dkt Jakaya Mrisho Kikwete,na Ali Hassan Mwinyi, pamoja na Rais John Pombe Magufuli, wakiweka shada la maua kwenye kaburi la Rais Mstaafu Marehemu Benjamin Mkapa.

Mkapa amezikwa kwa kuzingatia taratibu za imani yake ya Kikatoliki pamoja na taratibu za kiserikali ambapo amepigiwa mizinga ya kijeshi 21, ikiwa ni sehemu ya heshima kwa kiongozi huyo wa zamani.

Shughuli  ya mazishi ya kuhitimisha safari yake imefanyika katika viunga vya nyumbani kwao Lupaso, ambapo mamia ya wananchi miongoni mwao wakiwa ni viongozi waandamizi wa Serikali, wakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania pamoja na Marais wastaafu.

Mzee Mkapa anapumzishwa ikiwa imesalia siku moja tu, kati ya zile saba za maombolezo zilizotangwazwa na Rais John Magufuli, alipokuwa akitangaza kifo cha Hayati Benjamin Mkapa, usiku wa kuamkia Julai 24. 

Aidha Mzee Mkapa, anatajwa kuwa Rais wa aina yake kutokana na mageuzi ya kimfumo aliyoyafanya enzi za utawala wake (1995 -2005), ambapo pamoja na mambo mengine alianzisha taasisi mbalimbali za umma, ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA). 

Zaidi Mzee Mkapa katika upande wa Kimataifa anakumbukwa kama msuluhishi na mwanadiplomasia mahiri, aliyejitolea kuleta amani katika mataifa mbalimbali, ikiwemo Burundi.

Pumzika kwa Amani Rais wa awamu ya tatu, Benjamin William Mkapa.