Ijumaa , 27th Jan , 2023

Mkuu wa mkoa wa Mwanza Adam Malima, amepokea ripoti ya uchunguzi kuhusu tuhuma za kuuza viwanja vya serikali vinavyodaiwa kuuzwa shilingi bilioni 1 kinyume na taratibu na Mkurugenzi wa jiji hilo Selemani Sekiete, vilivyopo Halmashauri ya wilaya ya Nyamagana mkoani humo.

Selemani Sekiete, Mkurugenzi wa jiji la Mwanza

Akipokea ripoti hiyo, mkuu huyo wa Mwanza Adam Malima amesema kamati hiyo ya maadili imefanya kazi kubwa katika kufuatilia suala hilo na kuahidi kufanyia kazi yote yaliyoelezwa na kamati hiyo.

Aidha RC malima ameagiza kufuatilia migogoro yote ya ardhi katika mkoa huo kwani imekuwa tatizo linalojirudia kila mara kutokana na malalamiko ya wananchi anayopokea.

"Inaonekana kumekuwa unyang’anyi wa viwanja ndani ya Mwanza, kwamba mtu una kiwanja chako anakuja mtu mjanja kupitia idara ya ardhi na watendaji wake unanyang'anywa kiwanja chako its not fair na mara nyingi watu wanofanyiwa hivi ni watanzania wa hali ya chini na huenda ardhi ile ingekuwa ni jambo la manufaa kwake," amesema RC Malima

Awali akikabidhi ripoti hiyo Mkurugenzi wa Tume ya Maadili ya Viongozi kanda ya Ziwa Godson Kweka, amesema wakati wakikamilisha uchunguzi huo walibaini matatizo mengine ya ardhi na hivyo kuomba kuongezewa muda wa kufanya uchunguzi zaidi.

Kamati hiyo imetumia siku nane kuchunguza kuhusu uuzwaji wa viwanja viwili vya serikali namba 194 na 195 vinavyodaiwa kuuzwa kwa shilingi bilioni 1 na kupelekea hivi karibuni mkuu wa mkoa huo wa Mwanza Adam Malima kumshtaki kwa Ofisi ya Rais TAMISEMI Mkurugenzi wa halmashauri ya jiji hilo Selemani Sekiete kwa kuuza viwanja hivyo huku watumishi wengine wanne wakisimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa uuzwaji wa viwanja hivyo.