Jumatano , 3rd Jun , 2020

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika, amesema kuwa hawezi kuwazungumzia watu waliojitangaza kwenye vyombo vya habari kwamba, wanayo nia ya kugombea Urais kupitia chama hicho, ili hali mpaka sasa hivi bado hawajawasilisha barua zao ndani ya ofisi yake.

Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika.

Mnyika ameyabainisha hayo leo Juni 3, 2020, wakati akitoa tangazo la kwamba chama hicho kimefungua rasmi milango ya watia nia ya kugombea nafasi ya Urais kwa Uchaguzi Mkuu ujao, waanze kuwasilisha barua zao kuanzia leo hadi Juni 15, 2020.

"Utaratibu unaohusika na mchakato huu ni kuandika barua kwa Katibu Mkuu, tukishapata barua rasmi Kamati Kuu itakaa na kuwatafakari na kutoa mweleke, na wale ambao wametia nia kwenye vyombo vya habari na barua zao hazijafika kwa katibu Mkuu wa chama siwezi kuwazungumzia" amesema Mnyika.

Mpaka sasa hivi mtu aliyejitokeza kutangaza nia ya kugombea Urais ndani ya CHADEMA, ni mwanamama Dkt Mayrose Majinge, ambaye alitangaza nia hiyo siku za hivi karibuni mkoani Mwanza.