
Serikali ya Morocco imesema iko tayari kushughulikia malalamiko yanayochochea maandamano yanayoongozwa na vijana ambayo yameikumba nchi hiyo kwa siku kadhaa. Tangazo hilo limekuja siku moja baada ya watu watatu kuuawa na vikosi vya usalama wakati waandamanaji walipojaribu kuvamia kituo cha polisi.
Akizungumza na baraza la mawaziri siku ya jana Alhamisi, Waziri Mkuu Aziz Akhannouch alisema yuko tayari kwa mazungumzo na mijadala ndani ya taasisi na maeneo ya umma.
Wanaoshiriki katika kile kinachoitwa maandamano ya Gen-Z wanaishutumu serikali kwa ufisadi. Wameishutumu mamlaka kwa kutanguliza matumizi katika maandalizi ya Kombe la Dunia badala ya afya na elimu.
Vifo vya hivi majuzi vya wanawake wanane katika hospitali ya umma huko Agadir vimekuwa kilio cha kupinga kuzorota kwa mfumo wa afya wa Morocco.
Tangu yaanze siku ya Jumamosi, maandamano hayo yameongezeka na kuwa ya uharibifu zaidi, haswa katika miji iliyo mbali. Picha za mashuhuda zinaonyesha waandamanaji wakirusha mawe na kuchoma magari katika miji ya mashariki na kusini mwa nchi hiyo.