Jumapili , 15th Sep , 2019

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi watumishi saba katika Halmashauri mbili za Wilaya ya Kilombero, kwa tuhuma za ubadhilifu wa fedha zaidi ya Sh. Bilioni 1.3 za makusanyo ya mapato ya ndani.

Waziri Mkuu amewasimamisha kazi watumishi ha leo (Jumapili, Septemba 15, 2019) wakati akiongea na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero pamoja na watumishi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, akiwa katika siku ya pili za ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro.

Mbali na kuwasimamisha kazi watumishi hao, pia Waziri Mkuu ameagiza watumishi hao warejeshe fedha hizo ndani ya siku tatu kabla hajamaliza ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro. Watumishi hao ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Ifakara  Fransis Ndulane anayedaiwa  sh. milioni tano alizoingiziwa katika akaunti yake bila maelezo yeyote.

Amesema “Mkoa mzima wa Morogoro umekuwa na tatizo la upotevu wa mapato, fedha zinakusanywa zinapita mikononi mwa watu hazifiki benki, hii ni shida, hatutavumilia.”

Waziri Mkuu amesema kwa mujibu wa taarifa ya mkaguzi wa hesabu za Serikali (CAG) kipindi cha mwaka 2016 hadi juni 2019, Katika mji wa Ifakara  makusanyo yalikuwa ni bilioni 2.7  ambapo fedha iliopelekwa bank ni shilingi bilioni 1.9   na kwamba kiasi cha  shilingi milioni 727  hazijulikani zilipoenda.