Jumatatu , 30th Jan , 2023

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe, amesema kutokana na kuwepo kwa utapeli wanaofanyiwa Watanzania kwenye masuala ya kilimo, wizara hiyo imeanza kumfuatilia mtu anayejulikana kwa jina la Mr Kuku kwani imeshapokea malalamiko mengi kumhusu yeye.

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe

Kauli hiyo ameitoa hii leo Januari 30, 2023, Ikulu ya Dar es Salaam, na kuwaonya Watanzania kwamba hakuna kilimo cha WhatsApp, Instagram wala Twitter, na kusisitiza kilimo hakina njia ya mkato.

"Niwaambie walioko mijini, hakuna kilimo kinachoendeshwa kwa WhatsApp, Instagram wala Twitter, yaani msidanganywe ni kweli watu wengi wanaibiwa, tumeshashughulikia ishu ya JATU, na sasa tunamfuatilia mtu mmoja anaitwa Mr Kuku, tumeshapokea malalamiko mengi sana,"amesema Waziri Bashe 

Aidha Waziri Bashe amesema kuwa, "Acheni kulima kwa Twitter na WhatsApp, hamna mtu anaweza kukuambia lete milioni 10, baada ya miezi mitatu utapata milioni 15, niwaombeni ndugu zangu kwenye kilimo hakuna njia ya mkato, una hela yako kanunue ardhi ajiri kijana kutoka chuo kikuu, mweke shambani msimamie zalisha,".