Jumatatu , 11th Apr , 2016

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda ameitaka jamii sasa kuachana na huruma ya kutoa misaada ya fedha kwa watoto ambao wanarandaranda mitaani kwa kuomba fedha katika maeneo mbalimbali nchini.

Makonda ameyasema hayo baada ya kukerwa na idadi kuwa ya watoto wanavyozidi kuzagaa mitaani wakiomba huku wengi wao wakionekana kutumwa na wazazi au walezi.

''Watoto hawa ukitaka kumsaidia ukimwambia twende nikusaidie anakupiga chenga anaondoka maana yake ni kwamba wengine hutumwa na tukiendelea kuwapa fedha tunahatarisha maisha yao barabarani wanakozagaa'' Amesisitiza Makonda.

Aidha Makonda ameongeza kuwa kuwasaidia watoto hao kuombaomba ni kukuza taifa la vibaka wa baadaye na kuwafanya kutojishughulisha kwani wengi wao wana wazazi au walezi lakini hawapendi kukaa majumbani.

Hata hivyo amewataka wadau wanaopenda kusaidia watoto hao wawasaidie katika vituo maalumu na si kuwapa fedha mitaani jambo ambalo litawaweka katika mazingira salama kuliko ilivyo sasa.