Jumatano , 21st Aug , 2019

Mahakama Mwanzo mjini Morogoro imemuachia huru mtuhumiwa Even Mgaya (15) baada ya kukutwa hana hatia katika kesi ya uzembe na uzururaji inayowakabili watuhumiwa 29, na kuamuru kukamatwa kwa mwajiri wake ambaye ni mkufunzi wa Chuo cha Ualimu Kigurunyembe, aliyetambulika kwa jina la Mama Jak

Akihojiwa mbele ya Mahakama ya Mwanzo na Hakimu Emelia Mwambagi, mtoto huyo ameeleza kuwa sababu ya kukamatwa na polisi Agosti 16, 2019, ni kufuatia kutokuwa na mahali pa kwenda baada ya kufukuzwa na mwajiri wake.

Aidha mtoto huyo amefafanua kuwa amekuwa akiishi kwa mama huyo bila kupata nafasi ya kuwasiliana na familia yake, huku akidai kwa kipindi chote alichokuwa akifanya kazi hajawahi kupata malipo yeyote licha ya kuwa aliahidiwa kulipwa kiasi cha shilingi 40000 kwa mwezi.

Maelezo ya mtoto huyo yakapelekea Mahakama ikatangaza kumuachia huru wakati kesi ikiendelea ikiwa imejiridhisha kuhusiana na tuhuma zinazomkabili.

Baada ya kuachiwa huru kwa mtoto huyo hakimu Mwambagi akatoa hati ya kukamatwa kwa mama huyo siku ya leo Agosti 20 kwa tuhuma za kumfukuza mtoto Even mgaya na kuajiri mtoto mwenye umri wa chini ya miaka 18.

Hata hivyo Mahakama hiyo imeahirisha kesi ya msingi ya uzembe na uzururaji inayowakabili watuhumiwa 28, hadi Agosti 21 2019 kufuatia mashahidi wa upande wa mashitaka kutofika mahakamani.