Jumanne , 17th Apr , 2018

Mvua zinazoendelea kunyesha sehemu mbali mbali nchini zimeendelea kuleta madhara mkoani Rukwa, ambako zimeteketeza mashamba ya vyakula na kuharibu kabisa mazao.

Akizungumza na www.eatv.tv  Kamanda wa Polisi mkoani Rukwa, George Kyando amesema mvua hizo zimezoa kabisa mazao kwenye mashamba mkoani humo na mengine kuyafunika kwa udongo, hali ambayo imeleta hasara kwa wakulima.

Sambamba na hilo Kamanda Kyando amesema pia barabara mbali mbali zimekatika na kukosa mawasiliano kabisa, huku baadhi ya madaraja yakizolewa na maji, lakini hakuna tarifa ya vifo waliyoipata mpaka sasa.

“Huku Rukwa kuna barabara inayopita bonde kwa bonde kutoka mkoa wa Rukwa kwenda Katavi, kutokana na hizi mvua zinazonyesha madaraja yamechukuliwa na maji, bara bara imekatika, mashamba ya mipunga na mahindi yamefunikwa na udongo, kwa hiyo tumepata hayo majanga lakini tunashukuru Mungu hakuna mtu yeyote ambaye amedhurika na hiyo mvua, ni miundo mbinu na mashamba tu”, amesema Kamanda Kyando.

Kutokana na mvua hizo Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania imewataka wananchi kuwa makini wanaposafiri na kutembea, kwani mvua kubwa zaidi inatarajiwa kunyesha siku za hivi karibuni.