Jumatano , 4th Nov , 2015

Jeshi la polisi mkoani Tanga limemtia mbaroni mwanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Julius Joseph kufuatia kuwajeruhi wafuasi wawili wa chama cha wananchi (CUF) kwa kuwakata kwa kutumia shoka na panga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga Kamishna msaidizi wa Polisi Zubeir Mwombeji

Akielezea tukio hilo kamanda wa polisi mkoa wa Tanga Kamishna msaidizi wa polisi Zubeir Mwombeji amesema chanzo cha tukio hilo ni ushabiki wa kisiasa ambapo waliwekeana nadhiri kuwa endapo mmoja kati ya wagombea nafasi ya udiwani atashinda upande mmoja utalazimika kutoa ahadi hiyo.

Kufuatia hatua hiyo kamanda wa polisi mkoa wa Tanga kamishana msaidizi wa polisi Mwombeji amewataka wafuasi wa vyama vya siasa kuachana na ushabiki wa kufanyiana vitendo vya kikatili kwa sababu kuna maisha baada ya uchaguzi.

Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo wamesema mara baada ya mtuhumiwa kufanya tukio hilo kundi la wafuasi wa chama cha (CUF) walifanya vurugu kuashiria kutaka kulipiza kisasi hatua ambayo jeshi la polisi lililazimika kutumia nguvu ya ziada ili kuokoa maisha ya mtuhumiwa huyo ambaye aliingia kwa ajili ya kujificha katika nyumba ya msamaria mwema.