Jumanne , 7th Jan , 2020

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), mkoani Dodoma, inamshikilia mwanafunzi wa mwaka wa tatu, katika chuo kikuu cha St John's mkoani humo, James Kwangulija kwa kosa la kujaribu kutoa hongo ya laki tisa kwa afisa mitihani ili asaidie kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wenzake 6.

Akizungumza leo Januari 7, 2020, Mkuu wa TAKUKURU mkoani humo, Sosthenes Kibwengo, amesema uwepo wa tabia ya baadhi ya wanafunzi kutoa rushwa katika masomo, unapelekea kuzalisha wasomi wengi wasiokuwa na uelewa katika taaluma zao, hivyo kutokuwa na sifa za kuajiriwa kwenye soko la ajira hapa nchini.

"Leo tunatarajia kuwafikisha mahakamani watu wanne kwa makosa mbalimbali ya rushwa, akiwemo James Kwangulija (27), mkazi wa Kikuyu jijini Dodoma, mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa  shahada ya kwanza ya Ualimu katika chuo cha St John's kwa makosa ya kujaribu kutoa hongo ya laki 9 kwa afisa mitihani wa chuo hicho ili asaidie kuongeza GPA kwa wanafunzi wenzake 6" amesema Kibwengo.

Katika hatua nyingine TAKUKURU mkoani humo, itamfikisha pia mahakamani Rainer Kapinga, aliyekuwa Mganga Mkuu Wilaya ya Bahi, pamoja na Raymond Mhegele ambaye ni Afisa TEHAMA wa wilaya hiyo kwa kosa la matumizi mabaya ya madaraka yao.