Alhamisi , 30th Mar , 2023

Mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari Nyamilama Fadhili Maghembe,   amefariki dunia huku wanafunzi wengine 17 wakijeruhiwa kwenye ajali ya gari iliyotokea majira ya asubuh katika eneo la Gatuli kata ya Ng’undi wilayani Kwimba mkoani Mwanza.

 

Chanzo cha ajali hiyo kikitajwa kuwa ni mwendo kasi wa dereva ambapo gari hilo lilikuwa na wanafunzi 40 waliokuwa wakielekea Mwanza mjini kwa ajili ya likizo baada ya kufunga shule.

Mmoja wa wanafunzi waliokuwa katika gari hilo amesema gari lilimshinda dereva wakati akijaribu kukata kona baada ya kugonga bonde lililosababisha gari likose muelekeo na kwamba dereva huyo alikuwa mkaidi hata walipomsisitiza apunguze mwendo. 

Mganga mfawidhi wa hospitali  ya wilaya ya Kwimba Dk. Neema Gervas, amesema amepokea majeruhi 17 kwenye ajali hiyo huku mmoja akiwa amefariki dunia, na 12 kati yao wamepata majeraha makubwa huku wanafunzi wengine 6 wanafanyiwa uchunguzi wa mionzi .

"Wanafunzi 6 wamekwenda kwenye uchunguzi wa mionzi kwa sasa tunasubiri majibu ya X ray ili tuweze kujua hatua inayofuata pamoja na hapo tumeshatoa huduma ya awali ya dawa za maumivu na dawa za kuzuia tetenasi kwa wale wenye majeraha".

Mkuu wa wilaya ya Kwimba Ng’wilabuzu Ludigija, amefika katika hospitali ya wilaya ya Kwimba kuwajulia hali majeruhi wa ajaili hiyo na kutoa wito kwa madereva wote kuzingatia sheria za usalama barabarani kwa kuendesha gari kwa mwendo wa kawaida utakaomsaidia dereva kulimudu vizuri hata inapotokea dharura.