Alhamisi , 6th Oct , 2022

Mwenge wa Uhuru umemaliza mbio zake mkoani Kigoma, na kukabidhiwa mkoa wa Kagera huku ukiagiza wasimamizi wa Miradi ya Maendeleo Kila Halmashauri Nchini, kuwa wazalendo katika Kusimamia Miradi na kuleta ufanisi unaotakiwa kwa lengo la kusaidia maendeleo ya wananchi na Taifa

Ukiwa Mkoani Kigoma Mwenge wa Uhuru Umekimbizwa Kilomita 973 katika halmashauri nane za mkoa wa Kigoma, na kuzindua, kuweka mawe ya msingi na kutembelea miradi 51 yenye thamani ya Bilioni 12.03.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye akikabidhi Wakimbiza Mwenge Kitaifa kwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera amesema Mbio za Mwenge zimeacha manufaa makubwa katika miradi ya maendeleo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mheshimiwa Albert Chalamila akipokea Mwenge wa Uhuru kabla ya kuanza mbio zake ndani ya Halmashauri nane za mkoa huo amesema utapitia miradi 37 yenye thamani ya bilioni 13.6.

Katika Makabidhiano hayo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Sahili Geraruma ameagiza uwepo wa taarifa sahihi za miradi na kuagiza fedha za miradi ya vijana kuhakikisha inawakwamua kiuchumi.