Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara limethibitisha tukio la mauaji ya watoto wawili wa familia moja, Mwikwabe Saina (10), mwanafunzi wa darasa la tatu, na mdogo wake Joseph Saina (4), lililotokea katika Kijiji cha Rung’abure, Wilaya ya Serengeti mkoani humo. Chanzo cha tukio hilo kinadaiwa kuhusishwa na imani potofu za kishirikina.
Kwa mujibu wa taarifa ya polisi, tukio hilo lilitokea Februari 10, 2026 majira ya saa 11 alfajiri katika Kitongoji cha Getasamo, Kata ya Rung’abure. Inadaiwa watoto hao waliuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali na mtuhumiwa aliyetambulika kwa jina la Joseph Marwa (18), mkazi wa kijiji hicho.
Uchunguzi wa awali umebaini kuwa mtuhumiwa alimshutumu mama mzazi wa watoto hao kwa madai ya kujihusisha na vitendo vya kishirikina na kuwaloga ndugu zake, hali inayodaiwa kuchochea tukio hilo la kikatili.
Baada ya mauaji hayo, baadhi ya wananchi walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa na kuanza kumshambulia kwa fimbo na mawe kabla ya kuokolewa na Jeshi la Polisi. Kutokana na kipigo hicho, alipata majeraha makubwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Wilaya ya Nyerere (DDH) Mugumu kwa matibabu, ambapo baadaye alifariki dunia.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara linaendelea na uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo na limeeleza kuwa hatua stahiki za kisheria zitachukuliwa kwa mtu yeyote atakayebainika kuhusika.
Aidha, polisi wametoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na badala yake kutoa taarifa za uhalifu kwa vyombo vya dola ili hatua zichukuliwe kwa mujibu wa sheria.




