Ijumaa , 15th Dec , 2017

Katibu wa itikadi na uenezi wa Chama cha Mapinduzi CCM Ndugu Humphrey Polepole amevipiga kijembe vyama vya upinzani akimtaka mwenyekiti wa moja ya vyama hivyo kusema hela ziko wapi.

Kupitia ukurasa wake wa “Twitter” Polepole amendika maneno hayo bila kufafanua ni mwenyekiti wa chama gani na hela za nini japo wafuasi wake wengi katika mtandao huo wamechangia mawazo wakitaja huenda ni hela za ruzuku.

Mbali na hilo Polepole pia amesema kuwa kile alichowahi kukitabiri kuwa upinzani hawataweza kushindana na chama chake siku za baadaye kimeanza kutimia.

Hii inatafsiriwa kama majibu kwa mwenyekiti wa CHADEMA Mh. Freman Mbowe ambaye hivi karibuni alitangaza chama chake hakitashiriki uchaguzi mdogo wa Ubunge endapo Tume ya taifa ya uchaguzi (NEC) haitazifanyia kazi kasoro zilizojitokeza kwenye uchaguzi mdogo wa madiwani uliofanyika mwezi Novemba mwaka huu.

“Nalipata kuwaambia wataweka mpira kwapani, wakasubiri siku kadhaa na hatimaye imekuwa. Kwa lugha ya shule ya msingi miaka ile ningesema "wameogopa kuputa", wangeputa waone namna ambavyo kwetu siasa za masuala zinalipa. Ushauri wangu: "Mwenyekiti" lazima aseme hela ziko wapi”, ameandika Polepole.