Jumatatu , 16th Nov , 2020

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, kata ya Bagamoyo wilaya ya Kiteto mkoani Manyara, Charles Mbaluka, amerejesha kiwanja cha chama hicho alichokuwa amejimilikisha kinyume na utaratibu tangu mwaka 2015.

Mkuu wa TAKUKURU mkoani Manyara Holle Makungu.

Taarifa hiyo imetolewa hii leo na Mkuu wa TAKUKURU mkoani Manyara Holle Makungu, na kueleza kuwa uchunguzi ulibainika kwamba mwenyekiti  huyo kwa kuvunja maadili ya utumishi wa umma na chama chake alijimilikisha eneo hilo kwa kujenga nyumba yake na kuuza kipande kingine cha eneo kwa shilingi laki saba .

Hata hivyo mtuhumiwa alikiri kujimilikisha kiwanja hicho kinyume na sheria ambapo kiwanja hicho kitarejeshwa na kukabidhiwa kwa mkuu wa wilaya ya Kiteto Kanali Patric Songea, siku itakatayopangwa ili akikabidhi kwa viongozi wa CCM,kata ya Bagamoyo.

Aidha wametoa rai kwa viongozi wa CCM kuzitambua mali zote za chama hicho mkoani Manyara ikiwemo viwanja na kuhakikisha vinakuwa na hati miliki ili kuepusha kuporwa kwa mali hizo na viongozi wasio waadilifu.