Jumamosi , 18th Jun , 2022

Wananchi wa Kijiji cha Yakobi, Halmashauri ya Mji wa Njombe wamemkataa mwananchi mwenzao aliyefahamika kwa jina la mzee Gerhad Makinda kuishi kijijini hapo kutokana na tabia yake ya kupora mashamba kwa wananchi wenzie na kuwatolea lugha mbaya pindi wanapomhoji juu ya kufanya vitendo hivyo.

Mzee Gerhad Makinda

Kupitia taarifa ya Kijiji iliyosomwa na Mtendaji wa Kijiji hicho imeelezwa kuwa mwananchi huyo amekuwa si muungwana katika kuishi na watu kijijini hapo kwani inaelezwa kuwa amekuwa akichoma mashamba ya watu ambayo anataka kuyapora, kulisha mifugo yake katika mashamba ya wakulima mbwa wake kung'ata mifugo ya wananchi na yeye kukataa huku akiwatolea lugha za kuudhi.

Mkuu wa wilaya ya Njombe Kissa Kasongwa akiwa ziarani kijijini hapo akataka kuteua baadhi ya wazee maarufu kijijini hapo ili kukaa na Mzee Gerhad Makinda ili kujua ni kwanini analalamikiwa na wananchi lakini cha kushangaza wazee wote waliochaguliwa walikataa kukaa na mhusika kwa madai kuwa hawawezi kuelewana naye kulingana na tabia yake.

Baada ya kuona hali hiyo mkuu wa wilaya amesema kuwa mwananchi huyo ataitwa mbele ya kamati ya ulinzi na usalama ili ahojiwe ni kwanini anafanya vitendo hivyo vinavyochochea migogoro huku akiwataka wananchi kijijini hapo kuacha kuchukua hatua mkononi.