Jumatatu , 16th Jul , 2018

Mbunge wa jimbo la Mtama, Nape Nnauye amewasihi wakulima wa korosho wa mikoa ya Kusini kuikubali sheria mpya inayohusu tozo za zao hilo ambayo imepitishwa na Bunge.

Mbunge wa Mtama, Nape Moses Nnauye

Nape amesema hayo akiwahutubia wananchi wa jimbo lake katika mkutano wa hadhara Jumapili, Mei 15 ambapo amewaomba wakulima hao kwa sasa waikubali sheria hiyo na waipe imani serikali kama inavyosema kuwa sheria hiyo ina manufaa kwao.

Katika mkutano huo Nape amesema  "tunaidai serikali waitekeleze sheria yao waliyoipitisha kwa mwaka huu mmoja, baada ya hapo tutafanya tathmini kuona kama sheria yao imetufaa au haikutufaa".

Pia Nape ametumia mkutano huo kuwaondoa hofu wananchi wa jimbo lake juu ya taarifa zilizosambaa kuwa anataka kukihama chama hicho, akisema kuwa hana mpango huo kwa sasa kwa kuwa ana hisa nyingi ndani ya chama hicho.

Juhudi za kuwapata viongozi wa Bodi ya Korosho (CBT) waweze kuzungumzia kwa upande wao zimegonga mwamba kwa kuwa viongozi hao hawakutaka kuonesha ushirikiano.

Mwezi uliopita serikali ilipeleka Bungeni muswada kuhusu kuondolewa kwa tozo ya asilimia 65 ya usafirishaji wa nje wa zao hilo kutoka kwa wakulima kwenda kwenye mfuko wa hazina huku Bodi ya Korosho ikiidai serikali takribani shillingi billion 200, licha ya kupigwa vikali muswada huo ulipitishwa na wabunge na kuwa sheria rasmi.