Jumatatu , 4th Jul , 2022

Baadhi ya wakazi wa mkoa wa Kagera, wamelalamikia kupanda kwa nauli za Meli ya New MV. Victoria Hapa Kazi Tu, kutoka shilingi 16,000 hadi 21,000 kwa daraja la tatu, daraja la pili kutoka 30,000 hadi 40,000 na daraja la kwanza kutoka 45,000 hadi 55,000.

Meli ya New MV. Victoria Hapa Kazi Tu

Gharama hizo ni kwa wale wanaotumia Meli hiyo kutoka Bukoba hadi Mwanza, ambapo wananchi wamesema kwamba upandishwaji huo wa nauli ni mzigo kwao hasa kutokana na hali ngumu ya kiuchumi waliyonayo.

Wakizungumzia suala hilo la kupandishiwa nauli katika Meli hiyo pekee ya abiria ambayo ni tegemeo kwa wakazi wa mkoa wa Kagera, wamesema kuwa hatua hiyo itawagharimu kimaisha hasa wajasiriamali wadogo ambao wamekuwa wakisafiria meli hiyo kwenda kuchukua bidhaa mkoani Mwanza. 

Akitoa ufafanuzi kuhusiana na kupanda kwa nauli za Meli hiyo, afisa habari wa kampuni ya huduma za Meli yenye makao yake mkoani Mwanza, Fatna Msangi amesema kuwa, mabadiliko hayo yametokana na maelekezo kutoka Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) ambao waliwapa muda wa siku saba yawe yametekelezwa.